Pichani:Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Bi.Scolastika Njovu(kulia aliyevalia gauni nyeusi)akisalimiana na Bi.Esta Kambaulaya(Kushoto) wa Kijiji cha Magamba mara baada ya kutembelea makazi yake.Bi Esta amefanikisha ujenzi wa Nyumba anamoishi kwa sasa kupitia mpango wa TASAF.
Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ni moja kati ya Halmashauri zinazotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini TASAF.Mpango huu ulianza kutekelezwa rasmi Septemba mwaka 2014 ukiwa na walengwa 74 ukianzia utekelezaji wake katika Kijiji cha Magamba.
Mwandishi wa Makala hii ameelekeza jicho lake katika Kijiji cha Magamba Kilichopo Kata ya Magamba Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ambapo anakutana na mmoja wa wanufaika wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini TASAF Bi.Esta Kambaulaya na kuzungumza nae. Mazungumzo yao yanajikita juu ya namna ambavyo Bi.Esta ameweza kunufaika na mpango,na changamoto zake.
Bi Esta Kambaulaya(71) mkazi wa Kijiji cha Magamba anaeleza kwa kina namna ambavyo Mpango wa Kunusuru Kaya masikini TASAF umeweza kumsaidia kuboresha na kuendeleza shughuli zake mbalimbali za kilimo na namna ambavyo mpango huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kubadili maisha yake kutoka katika hali duni na hatimaye kwa sehemu kubwa kupunguza changamoto mbalimbali ikiwemo ya ugumu wa maisha .
Bibi Esta kama anavyosimulia alijiunga na mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF mwaka 2014 ambapo kabla ya kujiunga na Mpango anaeleza kuwa alikuwa akikabiliwa na hali ngumu ya maisha kwani alikuwa akitegemewa na mumewe ambaye alikuwa amekwishapoteza uwezo wa kufanya kazi kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya Kifua kikuu.
Licha ya kuwa Bi.Esta alijaaliwa kupata watoto 6 anaeleza kuwa hakuna msaada wowote kutoka kwa watoto wao kwa kuwa na wao pia wanaishi katika umasikini wa kutupwa na hakuna msaada wowote ambao anaupata kutoka kwao zaidi ya kuachiwa ulezi wa wajukuu watatu ambao wazazi wao wamekwishatangulia mbele za haki.
Baada ya kuingia kwenye Mpango kulingana na vigezo na masharti, alianza kulipwa kiasi cha Shilingi Elfu thelathini na sita 36000.Bi Esta anaongeza kuwa baada ya kupata kiasi hicho cha fedha aliamua kujikita katika ufugaji wa kuku ambapo alianza na kuku wanne.
Bi Esta alikuwa akiongeza idadi ya kuku kila mara alipopokea fedha na hatimae kuanza kunufaika na ufugaji wa kuku kutokana na kuuza mayai na kuku ambapo kwa sehemu kubwa aliweza kujikimu na familia yake
Baada ya kupata uzoefu wa kutosha katika ufugaji wa kuku mwaka 2016 Bi Esta alielekeza jitihada zake katika kilimo ambapo kwamwaka huo wa fedha aliamua kutumia kiasi cha fedha alichokuwa akikipata kununua pembejeo za kilimo na kuanza shughuli za kilimo cha Karanga.
Ni katika mwaka huo Bi Esta alifanikiwa kuvuna Magunia kumi ya Karanga ambapo gunia tano aliuza na kununua bati kwa ajili ya kuezeka nyumba yake ambayo kwa wakati huo ilikuwa imeezekwa kwa nyasi na gunia tatu aliuza na kununua mahindi kwa ajili ya kujikimu ambapo gunia mbili zilizobaki aliweka akiba ya mbegu kwa ajili msimu wa kilimo unaofuata.
Bi Esta kama ilivyo kwa wanufaika baadhi wanaotumia fedha za Mpango kwa kufuata maelekezo na ushauri unaotolewa na wadau mbalimbali wa TASAF anaeleza kuwa endapo fedha za Mpango wa Kunusuru kaya masikini TASAF zitatumika kama ilivyokusudiwa zitasaidia kwa kiasi kikubwa kubadili maisha ya wanufaika endapo tu watatumia kiasi kidogo wnachokipata kwa akili.
Amesema anaishukuru TASAF kwa kuwa Mpango huo umekuwa mkombozi kwake hasa anapokwama katika mahitaji mbalimbali ya kuendeleza shughuli zake za kilimo cha Mahindi Karanga na ufugaji.
Kwa sasa Bi.Esta licha ya kuwa hana msaada wowote kutoka kwa watoto wake anaeleza kuwa mpango wa TASAF umemkomboa kwa kuwa anayamudu majukumu yake kwa kiasi kikubwa.Anaeleza kuwa amefanikiwa kumlea Mumewe ambaye kwa sasa kama alivyokwisha sema awali kuwa hana uwezo wa kufanya kazi kutokana na kukabiliwa na maradhi ya Kifua.Pia Bi Esta anawapeleka shule wajukuu zake wawili ambao kwa sasa wanaendelea vema na masomo.
Bi. Esta anaeleza kuwa mafanikio makubwa zaidi yanaweza kufikiwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini TASAF endapo mpango huo utaboresha malipo kuendana na hali halisi ya kiuchumi.
Anatoa wito kwa baadhi ya wanufaika wa mpango huo kuhakikisha kuwa wanatumia kiasi hicho kidogo wanachokipata kwa kuingatia malengo mahsusi ya Mpango ambapo anabainisha kuwa kufanya hivyo kutawasaidia wao kujikwamua na hali duni ambayo iimewafanya wao kuingizwa katika Mpango huo.
Anatoa changamoto kwa wanufaika walioshindwa kutumia kiasi cha fedha za Mpango wa TASAF kuthubutu kujihusisha na shughuli za uwekezaji katika shughuli za ufugaji, na kilimo amabapo kufanya hivyo kutawasaidia wao kunufaika kikamilifu kama vile yeye alivyoweza kuboresha shughuli zake za ufugaji na Kilimo.
Kwa nafasi yake kama Mwanamke tena mwenye umri mkubwa anasisitiza kuwa endapo kila mnufaika akajituma kikamilifu itasaidia kwa kiasi kikubwa wao kutka katika Mpango huo na kuwapisha wengine ambao kwa namna moja ama nyingine hawakuweza kupata nafasi ya kuingia katika mpango.
Kwa sasa wanufaika wapatao 65 katika kijiji hiki cha Magamba wanaendelea kunufaika na Mpango wa Kunusuru kaya masikini TASAF ambapo kila msimu wa malipo unapifika Kiasi cha shilingi 1,684,000(Milioni moja laki sita na themanini na nne huelekezwa kwa walengwa hao na 100,000 hulipwa kama ruzuku ya kijiji.
Idadi kubwa kati yao wameweza kutumia kiasi cha fedha wanachokipata kuboresha shughuli mbalimbali za uzalishaji ikiwemo kilimo na ufugaji.
Idadi ya walengwa katika Magamba imepungua kutokana na vifo na wengine kuondolewa katika Mpango kutokana na sababu za kuwa katika uongozi.Aidha idadi ya Walengwa wa kijiji hiki cha Magamba wamepungua kutokana na sababu za kifo na kuhama na kufanya idadi yao kubakia 65 tafauti na walivyoanza.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : +255785659744
Simu: +255746310716
Barua pepe: info@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa