Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo wameombwa kutumia mikutano ya kisiasa kutoa Elimu na kuhamasisha Wananchi katika Kata zao juu ya umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii CHF Ulioboreshwa.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Bw.Mohamed Ramadhani katika kikao cha Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango kilichoketi 22 Desemba 2020 kujadili taarifa za Mwezi Novemba 2020.
Mkurugenzi Mohamed amewaambia Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kuwa Muitikio mdogo wa Wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii CHF Ulioboreshwa Nsimbo kumechangiwa pia kwa sehemu kubwa na Madiwani kutotumia Mikutano ya Hadhara kuhamasisha Wananchi kujiunga na Mfuko huo licha Halmashauri kujitahidi kuhamasisha.
Endapo Madiwani na Wataalamu katika ngazi ya Kata watashirikiana vema kuhamasisha Wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii CHF ulioboreshwa itasaidia kupatikana kwa fedha za kutosha katika Vituo vya kutolea huduma za Afya jambo litakalosaidia kwa sehemu kubwa kuimarika kwa huduma mbalimbali za Afya pamoja na upatikanaji wa Dawa kwa uhakika amesema Mkurugenzi Mohamed.
Mkurugenzi Mohamed Ameongeza kuwa ni vema wataalamu wa Afya katika ngazi za Kata wakashirikishwa katika mikutano ya hadhara inayofanywa na madiwani ili kuwapa fursa Wataalamu hao kujenga uelewa kwa Wananchi juu ya namna huduma za Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa zinavyopatikana kwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia Wananchi kuwa na uelewa na hivyo kupunguza malalamiko ambayo wakati mwingine yamekuwa yakisababishwa na Uelewa mdogo wa Wananchi kuhusu huduma zitolewazo na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa.
Aidha Mkurugenzi Nsimbo amewaomba Madiwani pia kushauri vema Bodi za Vituo vya kutolea huduma za Afya ili kuhakikisha kuwa Dawa zinazopendekezwa kununuliwa zinaakisi mahitaji halisi ya eneo husika ili kuepuka changamoto ya kutopatikana dawa katika baadhi ya maeneo.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : +2552955164
Simu: +255713992124
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa